Saturday, August 18, 2007

KUMUMUVUZISHA ZITTO KABWE KUMEMPANDISHA CHATI, SASA YUKO JUU


KUMUMUVUZISHA Zitto Kabwe, Kumempandisha Chati, sasa yuko Juu!!!!!



Kama Wabunge waliounga mkono Mh. Zitto Kabwe asimamishwe walifikiri wanamkomoa, basi hali ni tofauti kwani wananchi kibao wamemuunga mkono.


Baadhi ya Wabunge wakichangia mjadala wa kumsimamisha walisema anatumia Bunge kujipatia umaarufu wa kisiasa kumbe wenyewe ndio wanampatia umaarufu kwa kumtimua.Wananchi wengi wamechukizwa na kitendo cha kumsimamisha Kabwe kwani wanahisi ni janja ya kuwafunga midomo baadhi ya Wabunge wenye nia ya kweli ya kufichua maovu.


Kuanzia wasomi wa Chuo Kikuu (Profesa Mwesiga Baregu, mhadhiri mwandamizi wa masuala ya siasa na ushirikiano wa kimataifa wa UDSM) wamesikitishwa na uamuzi huo wa Bunge.Prof. Baregu alisema kwa kitendo hicho, Bunge halikumtendea haki Kabwe, halikutenda haki kwa demokrasia na pia halikutenda haki kwa wananchi.


Alisema kumwadhibu mbunge huyo hakujaweza kuondoa ukweli kwamba kuna mikataba mibovu inayoingiwa na serikali na suala la Buzwagi ni mfano tu kati ya mikataba mingi mibovu iliyoingiwa, hasa ya madini.


Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji Christopher Mtikila pia ameungana na wenzake akisema Zitto hana kosa, adhabu aliyopewa ni uharamia wa demokrasia na suala ambalo kila Mtanzania anatakiwa kulitambua na kutotakubali kukaa kimya.


Naye Wakili wa Kujitegemea, Tundu Lissu, alisema adhabu iliyotolewa kwa Kabwe sio halali, huku akitaka mbunge huyo aruhusiwe kuendelea na vikao vyote vya Bunge.Akiongea kwa niaba ya Asasi za kiraia Lissu alisema ni bora Bunge likaeleza mbunge huyo amepewa adhabu ya ngapi ili wananchi walinganishe na kufahamu adhabu ambayo ilikuwa inastahili kulingana na kosa, kama analo.


Wengine waliohojiwa wamesema uamuzi huo ni sawa na kuwanyima haki wapiga kura wa Kigoma Kaskazini kwani watakosa mwakilishi kwa kipindi alichosimamishwa.Hivi sasa Mbunge huyo anawasiliana na baadhi ya wanasheria kuona uwezekano wa kukata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga adhabu hiyo.


Na katika kumwuunga mkono CHADEMA wanaandaa mapokezi ya Mbunge wao huyo pindi atakaporejea Dar akitokea Dodoma alikomuvuzishwa nje ya Bunge hadi Januari mwakani.


Huko Dodoma nako Wabunge wa upinzani wamekaa kikao cha dharura kutafakari cha kufanya baada ya mwenzao Kabwe kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge.Na katika kumuunga mkono Wabunge hao wa upinzani wamesema kuwa kila mwezi watakuwa wanamchangia karibu sh. milioni 1.5/- ili afanikishe kazi zake anazofanya za Ubunge.Katika adhabu aliyopewa Mbunge huyo atakuwa analipwa nusu mshahara hadi atakaporejea tena Bungeni kuendelea na vikao.