Monday, September 21, 2009

MAPENZI hayana umri jamani, hebu msome mzee wa miaka 70 aliyejinyonga kwa wivu wa mapenzi!

Na Martha Mtangoo, Dodoma

9/21/2009

MZEE wa miaka 70 aliyefahamika kwa jina la Msuliche Mhogo amejinyonga kwa kutumia kamba kutokana na wivu wa mapenzi.

Kamnda wa polisi mkoani hapa Zelothe Steven aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 asubuhi katika kijiji cha Ngh’ambi wilayani Mpwapwa.

Akielezea tukio hilo Kamanda Zelothe alisema kuwa chanzo cha mzee huyo kujinyonga ni kutokana na wivu wa kimapenzi kwa mkewe mwenye umri wa miaka (30) ambaye jina lake limehifadhiwa.

Alifafanua kuwa kwa muda mrefu mzee huyo alikuwa akihisi mkewe ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine hapo kijijini ambaye ni jirani yake.

Alisema kuwa awali kabla ya tukio hilo kutokea , usiku mzee huyo aligombana na mkewe kuhusu mtoto wao mmoja ambaye ana umri wa miaka miwili akidai kuwa mtoto huyo ni wa mwanaume ambaye nahisi anatembea naye na si mwanaye.

Kamanda Zelothe alisema kuwa wakati wakiendelea na ugomvi huo mke mkubwa wa mzee huyo alienda kuamua ugomvi huo na ilipofika asubuhi mzee huyo aliaga kuwa anaenda safari na ndipo alipokwenda kwenye mbuyu ambao upo jirani na nyumbani kwake na kujinyonga.

Wakati huohuo jeshi la polisi mkoani hapa linamshikilia Hamis Salum (27) mkazi wa Manispaa ya Moshi kwa tuhuma za kufungua duka na kuiba simu 10 za aina mbalimbali.

Kamanda Zelothe alisema kuwa baada ya kufungua mlango mtuhumiwa huyo alijfungia ndani ya duka hilo na kuanza kukusanya simu dukani humo ambapo mwenye duka ambaye ni Freeman Narcis (23) alifika dukani hapo na alipofungua duka alimkuta mtuhumiwa huyo akiendelea kukusanya vitu katika duka hilo .

Kamanda Zelothe alisema kuwa jeshi hilo bado linamshikilia mtu huyo kwa mahojiano zaidi na atafikishwa mahakamni mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Ends……