Friday, June 13, 2008

BAJETI 2008/2009, SERIKALI imeshindwa kupunguza bei ya mafuta!


SERIKALI imeshindwa kupunguza bei ya petroli na dizeli katika bajeti yake ya mwaka 2008/2009, badala yake imewabana wavuta sigara na wanywaji wa bia na soda kwa kupandisha kodi ya bidhaa hizo.
Pamoja na kutoongeza ushuru katika bidhaa za petroli, bado wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaona hali itaendelea kuwa ngumu katika sekta za uzalishaji na usafirishaji kutokana na kuongezeka kwa kasi bei ya nishati hiyo katika soko la dunia, hivyo wananchi kuendelea kuishi katika hali ngumu katika kipindi cha mwaka huu wa bajeti.
Bajeti hiyo pia imeongeza ushuru wa bidhaa katika huduma za simu za mkononi kutoka asilimia saba ya gharama ya matumizi ya huduma hadi asilimia 10. Kwa mantiki hiyo, gharama za matumizi ya simu zitaongezeka kwa watumiaji.
Akiwasilisha, mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2008/2009 bungeni jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo hata hivyo, alitangaza kufutwa na kupunguzwa kwa kodi kadhaa zikiwemo za pembejeo za kilimo na ushuru wa magari, gesi na mafuta ya viwandani.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, vinywaji baridi vimeongezwa ushuru kutoka Sh48 kwa lita hadi Sh54, bia inayozalishwa Tanzania ambayo haijaoteshwa imepanda kutoka Sh173 kwa lita hadi Sh194, bia nyingine kutoka Sh 294 hadi Sh 329 na mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu iliyozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka Sh940 hadi Sh1,053.
Bidhaa nyingine zilizopanda bei ni vinywaji vikali kutoka Sh1,394 kwa lita hadi Sh1,561, sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa nchini kutoka Sh4,775 hadi Sh5,348 kwa sigara 1,000; sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kutoka Sh11,266 hadi Sh12,618 kwa sigara 1000, sigara nyingine zimepanda kutoka Sh20,460 hadi Sh 22,915 kwa sigara 1,000 na tumbaku iliyo tayari kutengeneza sigara pia imepanda bei kutoka Sh10,333 hadi Sh11,573 kwa kilo.
Aidha, serikali imefanya marekebisho ya kodi ya kima cha chini cha mshahara na kutangaza kwamba kuanzia sasa mshahara usiozidi Sh100,000 hautatozwa kodi. Awali, kima cha chini kilichokuwa hakitozwi kodi kilikuwa Sh80,000.
Hata hivyo, wafanyakazi wanaopata mshahara wa zaidi ya Sh720,000 wameongezewa kodi na sasa watalipa Sh120,000 kuongeza asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh720,000.
Akizungumzia bidhaa zilizofutiwa ushuru, Mkulo alisema kwamba serikali imesamehe ushuru wa forodha kwenye majembe ya mkono pamoja na pembejeo nyingine zote za kilimo zinazoagizwa kutoka nje ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wakulima hasa wale wadogo.
Alisema uamuzi wa kusamehe kodi hiyo upo katika mapendekezo ya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha yaliyojadiliwa pamoja na na nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi katika kikao cha maandalizi ya Bajeti cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Juni 2, 2008 Jijini Nairobi.
Kodi nyingine iliyofutwa ni ya lami ambayo kwa mujibu wa Mkulo,
imelenga kupunguza gharama za ujenzi wa barabara, mafuta mazito yanayotumika kama nishati ya kupikia kama Moto Poa, gesi asilia iliyosindikwa na mitungi ya kuhifadhia gesi hiyo, kama ilivyo hivi sasa kwa gesi ya kupikia ya LPG, ili kuhamasisha matumizi ya gesi hiyo badala ya mafuta ambayo ni ghali, au mkaa ambao unaharibu mazingira.
Pia serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye magunia yanayotengenezwa hapa nchini kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa magari yaliyotengenezwa maalum kwa ajili ya ukusanyaji takataka yatakayonunuliwa na Serikali za Mitaa au mawakala walioidhinishwa na Serikali za Mitaa.
Mkulo alisema serikali imeondoa ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya kula. Lakini mafuta yaliyosafishwa kidogo yataendelea kutozwa ushuru wa asilimia 10. Alisema hatua hiyo itaviweka viwanda vya mafuta nchini katika nafasi nzuri ya kiushindani na vile vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia imepunguza ushuru wa mafuta mazito ya HFO, kutoka Sh117 kwa lita hadi Sh97 ili kupunguza gharama za uzalishaji viwandani na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko.
Kuhusu kodi za magari, Waziri huyo alisema kwamba serikali imepunguza ushuru wa magari kutoka asilimia 10 kwa magari yenye ukubwa wa injini unaozidi cc2000 na kuwa na viwango viwili vya asilimia tano na asilimia 10.
Katika mabadiliko hayo, magari yenye ujazo wa injini usiozidi cc1000 hayatalipiwa ushuru wa bidhaa huku yale yenye ujazo wa injini unoazidi cc1000, lakini hauzidi cc2000, yatalipa ushuru wa asilimia tano ya thamani ya gari, na magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc2000 yatalipiwa ushuru wa asilimia 10.
Mkulo alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kukusanya Sh7,216,130 bilioni na kutumia asilimia 64 ya bajeti yote kushughulikia miundombinu ya uchumi na huduma za jamii.
Matumizi ya serikali kwa mwaka 2008/09 yatakuwa Sh7,216.130 bilioni ambayo ni jumla ya matumizi ya kawaida ya Sh4,726.650 bilioni na matumizi ya maendeleo ya Sh2,489,480 bilioni.
Alisema serikali pia imetenga fedha kwenye maeneo muhimu kwa kuzingatia vipaumbele na mipango ya kitaifa ambayo ni Elimu iliyotengewa Sh1.43 trilioni, Miundombinu ya barabara Sh973.3 bilioni, afya Sh 803.8, Kilimo Sh460.0 bilioni, maji Sh 230.6 bilioni na Nishati Sh383.4 bilioni.
Mbali na maeneo hayo pia kuna fedha zitakazotumika kutekeleza Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) katika nyanja za utawala bora, ulinzi na usalama, malipo ya madeni, pensheni na Bima ya Afya.
Waziri Mkulo alitaja kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, nafaka, pembejeo za kilimo na malighafi za viwandani kuwa changamoto zitakazoikabili bajeti ya mwaka huu ingawa serikali imejipanga vizuri kukabiliana na changamoto hizi.
Alisema ongezeko la bei ya bidhaa hizo limesababisha kasi ya mfumuko wa bei karibu katika kila sekta na kuvuruga masoko ya fedha ya kimataifa jambo ambalo limeathiri mtiririko wa vitega uchumi (FDI) kutoka nchi tajiri kuja nchi maskini
Changamoto nyingine ni kuongeza mapato ya ndani na kudhibiti kukua kwa haraka kwa bajeti ya kawaida, ili kuanza kujitegemea.
Alisema utegemezi wa bajeti kwa wahisani ni tatizo kwani michango na misaada yao haifiki kwa wakati hivyo kuna haja serikali kupunguza kasi ya kuongezeka kwa matumizi ya kawaida, hasa yale yasiyoweza kurekebishwa iwapo mapato yatapungua.
''Kwa hiyo, kunahitajika umakini mkubwa katika kuhimili athari za hali hii ya uchumi wa dunia. Hata hivyo, nchi zinazozalisha mafuta ya petroli zinategemewa kuendelea kunufaika na ongezeko la bei ya mafuta hasa kwa kuwa mahitaji ya nchi kama China, India na Brazil ni makubwa,'' alisema.
Hata hivyo, alisema serikali imeandaa mikakati kadhaa ya kukabiliana na hali hiyo ikiwamo kupunguza utegemezi kutoka asilimia 42 mwaka jana hadi asilimia 34 mwaka huu.
Alisema pia serikali itahakikisha upatikanaji wa nafaka ambazo bei zake zinapanda kwa kasi na kuathiri maisha ya wananchi na kusitisha usafirishaji nje wa bidhaa hizo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri vijijini, ili kupunguza gharama za kusafirisha chakula hadi kwenye maeneo ya soko.
Alishauri kutumia ongezeko la bei ya chakula duniani kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula nchini, kwa kuhimiza kuwekeza katika mashamba makubwa na kuhimiza wananchi walime chakula kwa wingi ili kujipatia chakula na kipato.
Lete maoni yako kuhusiana na Bajeti ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2008/2009 karibu saaaana!