Saturday, December 10, 2005

Hii ndio Hali halisi ya Wabongo!!!!!





HII ndio hali halisi ambayo inatukuta wabongo wengi hapa kwetu, kagari kadogooo lakini watu kibao, utadhani marobota ya Pamba yanasafirishwa toka shinyanga kwenda Dar es salaam kwenye kiwanda cha kutengenezea Nguo.

halafu mbaya zaidi gari hii ikakosa mafuta na kuna watu wana haraka zao wengine wagonjwa, wengine wanawahi Benki kuchukua hela kwa ajili ya kununulia mahitaji yao na mbaya zaidi siku yenyewe ni ya Jumamosi ambayo ni nusu siku!

safari moja huanzisha nyingine, yalishamkuta Mgombea urais Mwanamke Pekee , Komando Anna Senkoro mara Wese si likamuishia!!!!!!!!!!!!!!!!! basi bwana akaanza kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua Mafuta kama CHAMA CHA MADAKTARI WANAWAKE (MEWATA), wanavyoomba kuchangiwa fedha kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa akina mama!

sasa mbaya zaidi ni kwamba pamoja na gari hili kujaza watu kibao babaake! sheli hakuna wese wala nini ili kuepuka usumbufu kwa wafanyakazi kuulizwa mafuta yapo? wameamua kuweka Bango Kubwaaaaaaaaa, Eti NO FUEL! UNGEKUWA WEWE NI MMOJA WA ABIRIA KATIKA GARI HII UNGEFANYAJE?

Nakaribisha maoni, changia bila jazba wala upendeleo!

Friday, October 28, 2005

AKIFA Mwingine uchaguzi si utafanyika 2006? Mrema naye Hoi kitandani!

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jana imetangaza kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kufuatia kifo cha aliyekuwa Mgombea urais Mwenza wa CHADEMA kufariki dunia.

NEC imetangaza tarehe mpya ya uchaguzi kuwa nui Desemba 18 mwaka huu kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni.

nilipopata tarifa hizo jana nilishtuka sana kwa maana kwanza huyo mgombea mwenyewe ukweli nilikuwa simfahamu kabisa kwa jina wala kwa sura, ushanipata bwana?

unajua kitu gani kimenishtua ni hiki: uchaguzi umeahirishwa hadi Desemba 18 mwaka huu, eti mpaka CHADEMA wateue mgombea mwenza mwingine wamnadi halafu ndo watu wampigie kura!

unajua inachekesha sana, panapochekesha ni hapa: huyo marehemu mwenyewe ni watu wangapi walikuwa wanamfahamu? na je huyo atakayeteuliwa atapa kura ngapi?

haya muda nao sasa akifa mwingine itakuwaje? maana mrema naye ambaye ni Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha TLP ni mgonjwa hoi bin taaban kitandani! kwa kweli tume imenichanganya sana.

kwanza wagombea wenyewe wamechoka na kampeni, lakini pia hata sisi wananchi pia tumechoka, cha msingi sasa ni mara bunge litakapopatikana itabidi libadilishe sheria zote zilizopitwa na wakati ikiwemo hii sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 maana imenichefua sana.

zisiporekebishwa Serikali yenyewe itajikuta siku moja inajifunga na sheria iliyotunga yenyewe na mbaya zaidi mpaka sasa jumla ya sh. bilioni 43 zimeshatumika kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi, ambapo jumla ya sh. bilioni 93 zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi huo ambao sasa utafanyika Desemba 18.

Mimi nimechoka sana na siasa za inji hii sijui nyie wenzangu mnazionaje?

Thursday, October 13, 2005

Kha! Kumbe Nchi Imeshaposwa? Wenye Nchi tunafanyiwa Kicten Party Sasa!!

HAKI ya Mungu sasa Tanzania tunakoelekea kubaya sasa, Ni jana tu nilikuwa nasoma Blog ya Bw. Msangi nikakutana maoni ya Watu wengi sana kuhusiana na Matunda ya Uhuru ambaye kwa sasa yamegeuzwa Matundu ya Uhuru!

kilichonishtua zaidi baada ya kusoma maoni ya msomaji mmoja ambaye alisema kwa sasa Tanzania imeshatolewa Posa na Wawekezaji toka nje ya Nchi ambao kabla ya kuioa Tanzania bado wanaifanyia Kitchen Party!

Mbaya zaidi waowaji hao wanakuja na mashartimagumu sana kwa waolewaji jambo ambalo linawakandamiza sana waolewaji lakini cha kujiuliza ni hiki je ni Kweli Tanzania haina uwezo wa kutafuta vitendea kazi vyenye ubora wa kimataifa na kufanya kazi zake yenyewe na kuwauzia haoa hao wanajiita wawekezaji?

Najisikia hasira sana ninapoona Mkurugenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita ni Mzungu wakati kuna watanzania ambao wana uwezo wa kufanya kazi hiyo ya Ukurugenzi katika Mgodi kama huo.

Sasa sisi watanzania ambao tunafanywa Mali Ghafi tufanye nini ili Tusikandamizwe na hawa waowaji wenye masharti Makali namna hii?

Sunday, September 11, 2005

Mzee wa Miaka 85 kuhutubia Umoja wa Mataifa, Yuko Darasa la Pili

AMA kweli Elimu haina Mwisho, kwa hili unaweza ukaamini kwamba ni kweli sasa hii ni karne ya Sayansi na Tekonoljia na Si zama za mawe za Kale.
Enzi za ujana wetu miaka ya 47 hakukuwa na kitu kama hiki na wala utamaduni kama huu haukuwepo wa kikongwe kusoma ete anaanza darasa la kwanza akiwa na miaka 84 haya ni maajabu! tena ya Musa.
sasa hebu hapa uhondo kamili hapa

Saturday, August 20, 2005

Nikusikie tena unatishia watu Amani!


Inasemekana Vyama vya upinzani vinafanya fujo makusudi kutokana na wagombea wa Vyama hivyo kujua kuwa havitashinda katika uchaguzi Mkuu ujao.

Lakini kwa mujibu wa Wachunguzi wa masuala ya Siasa wanasema kuwa ni katika kujitetea tu ndio maana vyama hivyo vinafanya hivyo,

Je wewe Msomaji wa Blog hii una maoni gani? unafikiri ni kwa nini inakuwa hivyo? weka maoni yaklo hapa ili unisaidie kuelewa ni kitu gani kifanyika na kwa malengo hani hasa, unakaribishwa kuweka hoja zako bila jaza wala upendeleo wa aina yoyote.

Karibuni.

Tuesday, August 16, 2005

Ni kama anasema "Ndejembi Mwenzio najisikia Kizunguzungu nisaidie ninyanyuke hapa nisije nikaanguka!" Huyu Makamu Mwenyekiti wa CCM na Muasisi wa CCM Mzee Rashid Mfaume Kawawa ambaye jana alishindwa kuendelea kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM almaarufu NEC kutokana na kuugua ghafla akiwa ukumbini. Mzee tunalkubali mchango wako saaana lakini pumzika sasa umechoka he! unataka kufa kishujaa?
Kwa habari zaidi Soma hapa.

Wednesday, August 03, 2005

HAYA TENA MABLOGST WANAZIDI KUONGEZEKA!!!!!

Ni waandishi wa Habari tu tena toka Dodoma, huyu nae ni Mpiga Picha wa ITV Dodoma naitwa Twaha kivale, Bonyeza hapa umsome.

Tuesday, August 02, 2005

Si Ulitaka Chai! Iweje ulalamike Unaungua?



Baada

Haya Jamani tukiambiwa tuache kunywa Chai kavu tunang'ang'ania Tu na Matokeo yake ndo haya Tunaungua, Kunywa chai na Vitafunio hata ikiwa ya Moto Kiasi gani huwezi Kuungua kama ilivyomuunguza marehemu Mrembo Huyo ambaye alikuwa akisoma Chuo Kikuu cha MOI huko Nchini Kenya.

Alipojijua kama ameambukizwa Virusi ya Ukimwi akaahidi Kulipiza Kisasi kwa yeyote ambaye atakatiza Machoni Mwake na alifanikiwa kuambukiza Jumla ya Wanaume 124 nchini humo ambao waliopona ni 6 kwa kuwa walimua kunywa chai na Vitafunio.

Kabla alikuwa Mrembo sana kama anvyoonekana katika Picha ya Chini
Nawaombeni sana Radhi Wapenzi wasomaji wa Blog yangu, kwa kuchapisha Picha ya Kutisha namna hii hii inasababishwa na Mimi kuguswa sana na Tukio hili.
Kunyweni Chai na Vitafunio Jamani la Sivyo Tutaungua!

Wednesday, July 27, 2005

KHA! Akina dada Tumelaaniwa au?


NAJUA, kuwa kila mtu anayetyembelea Web Page yangu anafahamu kuwa ni nini naongelea zaidi katika kila kurasa.

Sasa hili nililokutana nalo linaniytia uchungu sana, inaniuma sana ninapoona akina dada wenzangu wanafanya mambo ya ajabu wakati wamejaaliwa kila kitu yaani wamekamilika kila Idara.

Hebu angali sasa ni nini hiki? inaiuma sana kuona akina dada hatujithamini kabisa miili yetu, eti siku wanasema wapewa bure na lazima wapewe bure wewe usijidanganye kwa hilo na ulaaniwe.

Huyu ukimuuliza ni nini anafanya hapo atakwambia yuko kazini lakini hiyo kazi yako ya kucheza shoo ukivaa vizuri mbona itanoga tuuu? kilichomsibu sasa Soma hapa chini.


Mr Nice nusura amtwange mnenguaji wake!

MWANAMUZIKI mahiri katika miongoko ya Takeu ya kizazi kipya Lukas Mpenda almaarufu Mr Nice Ijumaa iliopita alimkwida mnengaji wake aliyetambulika kwa jina la Mpasi Mussa nma almanusura angemtwanga makonde.

Tukio hilo lilitokea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bendi ya Msondo Ngoma Music ambayo zamani ilikuwa ikiitwa OTTU Jazz. Mr Nice alimkunja mnenguaji wake akionekana kapndwa na hasira kitendo kilichofanyika nyuma ya jukwaa la ukumbi huo uliokuwa umehudhuria na mashabiki wengi.

Mr Nice alizua tafrani hiyo kwa madai kwamba mnenguaji wake huyo alikosa nidhamu kwa kudai pesa yake kwa utaratibu aliodai haukuwa wa heshima. "Inabidi nikuonye kutokana na utovu wa nidhamu ulioufanya, nakuonya kama mdogo wangu," alisikika akifoka Mr Nice.

Hata hivyo menguaji huyo aliomba msamaha na ndipo Mr Nice alipomwachia huku akisikika akimwambia: " Mimi sipendi kufanya kazi na watu kama nyinyi, sitaki kuwa pamoja na wewe kwa sababu umenidhalilisha."

Acha kazi kwani lazima ucheze Shoo? anza hata kuuza Vitumbua au Maandazi ukiwa na Msimamo maisha yatakunyookea mwenyewe utashangaa huwezi kuamni.

Haya kila la Kheri

Monday, July 18, 2005

Wizara Nyeti ambayo Waheshimiwa Wabunge hawaifahamu!!!


WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII

WIZARA ya Maliasili na Utalii ni Wizara NYETI ambayo watu wengine bado hawajatambua Unyeti wa Wizara hii, inaniuma sana.

Nafikiri kila mtu anajua ni kwa nini hilo linaniuma saaana, Utamaduni wetu watanzania ni pamoja na mali ya asili ambayo ni Misitu na hifadhi za wanyamapori.

Naumia sana kwa maana Utalii ni pamoja na Wanyamapori, Milima, Maziwa na Mito ambayo ipo hapa Tanzania.

Sasa hebu fikiria kinachonisikitisha zaidi ya yote ni kwamba hata Waheshimiwa Wabunge wenyewe wa Bunge la Jmhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (TANZANIA), hawajui kabisa kuwa Wizara hii ni Nyeti.

Utajuaje kama hawajui kuwa Wizara Nyeti sio Nyeti, ni hivi kwanza Wizara hii haina msaidizi kabisa, Mwanamama
ZAKIA HAMDANI MEGHJI anafanya kazi Mwenyewe kama Waziri wa Malisili na Utalii.

Ni kwamba wabunge walishindwa kushinikiza kuwa Wizara hiyo Nyeti iwe na Msaidizi yaani hapa naamnisha kuwa Wizara hiyo haina naibu waziri.

Mama huyu pamoja na kutokuwa na Naibu Waziri kama ilivyo wizara nyingi tu ambazo zingine zina manaibu Waziri watatu kama ilivyo Wizara ya Fedha anafanya vizur sana.

Angalia Watalii wameongezeka kutoka 295,312 mwaka 1995 hadi kufikia 582,807 mwaka 2004, hii ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 10 kwa mwaka.

Hali kadhalika mapato yatokanayo na utalii yameongezeka toka dola za kimarekani milioni 259.4 mwaka 1995 hadi Dola milioni 746.0 mwaka 2004 mabpo mpaka mwaka huo Sekta hiyo ilikuwa imetoa ajira kwa watu wapatao 199,000.

Sasa kwa nini mama huyu ambaye anautangaza utamaduni wa Mtanzania nje ya Tanzania asiwe na Msaidizi? Haya nikisema utasikia ooh wanawake bwana wanataka dezo hatutaki dezo na kazi tuweza sana, Hongera sana Mama Meghji kwa kazi nzuri.

Lakini ni vyema Serikali ya awamu ya nne ikazingatia ushauri huu kuipatia Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kuwa hii ni Wizara Nyeti kama zilivyo wizara nyingine ikiwezakana atoke Wizara ya Fedha azibe nafasi hiyo.

Angalia utalii wa Tanzania hapa uvayotangazwa bila upendeleo hiyo ikiwa ni kazi ya Mwanamama na mwaka huu anagombea hataki viti maalum tena!!!!!!!

Monday, July 11, 2005

Inapofikia hatua Mtoto Anazaa Mtoto Mwenzie!! What has become of mankind?

Ama kweli sasa tulipofikia ni Karibu na Mwisho, Hivi Yesu atarudi lini? kila mtua ana majibu yake wengine wanasema alisharudi wengine wanasema arudi kufanya nini yote Kheri lakini na tumuombe sana atausaidie kuelewa.

Hii ni picha ya Mtoto mwenye umri wa miaka 10 tu! wa Wilaya ya Kericho Nchini Kenya, kila mtu atauliza sasa kma wa Kericho Nchini Kenya si tufanyaje, Sikiliza ni Mtoto wa miaka 10m ambaye miezi michache iliyopita alikuwa akicheza na wenzie michezo mbalimbali akirudi Nyumbani anaogeshwa lakini sasa amekuwa mama wa Mtoto Jamani tunaenda wapi?!

Kinachoniuma zaidi ni kwamba Baba Mtu mzima ana akili zake ameamua kumfanyia hivi huyu mtoto mdogo ambaye ni sawa na mwanaye wa kumzaa jamani inatia uchungu sana sijui ni wapi tunaelekea Mungu tusaidie kuelewa nini Tunatenda.

Inauma sana, inakatisha tamaa, hebu fikiria mtoto mdogo namna hii anamnyonyesha mtoto mwenzie amezaa anaweza kulea? anaweza kujua iwapo leo mwanangu anaumwa sasa nimpeleke Hospitali? wewe Baba Jitu Zima umemtafutia matatizo ambayo yanamfanya mtoto anaingia katika kitabu cha historia wewe umepumzika.

Ukimuuliza alikuwa anatafuta nini kwa mtoto mdogo tena bado ananuka Shombo kali madai yake mtoto mdogo hana Ukimwi, hatakuwa na ukimwi wakati mizee mizima inataka watoto wadogo?

Na Walaaniwe wote wenye tabia mbaya inayomsababishia mtoto mdogo matatizo katika Siku zote za Maisha yake.
Unakaribishwa kuchangia Bila Jabza wala Upendeleao wa Kijinsia Karibu.

What has become of mankind?

This is a picture of a 10 year old lovely school girl,from the Kericho District in Kenya.
What makes her sospecial? With her whole life ahead of her, a wonderful futureto strive for an education and to move into her teenyears and have fun playing with her fellow girls,children of her own age, she is not playing withdolls.
She is handling the real thing. She has becomea Mother.
Definitely there is a Man somewhere who is to blame!What has become of mankind?People have no fear of the Creator, the Most Merciful,the most Benevolent.
Are we coming to the end?

Tuesday, July 05, 2005

Kwa Nini Sisi Tuweze tuna Nini na Nyie mshindwe mna nini? Mnannisikitisha sana, nyingine mpya hii hapa!!!!!!


NASIKITIKA sana kuona eti asilimia 95 ya Mablogist wa Kiswahili ni Waandishi wa Habari kwa nini lakini?

Mbona mnaifanya mioyo yenu kuwa migumu jamani, Kublog kiwahili sio dhambi, na kama siyo dhami haiwezi kuleta mauti zaidi ya kukupatia faida jamani kwa nini?

kama mnadhani mimi muonugo Fungua Blog nyingine hii hapa www.ngurumo.blogspot.com uone nini kunaendelea.

huyu anaitwa Ansbert Ngurumo ni Mwandishi wa habari Mwandamizi na Nzuri zaidi ni Mhariri wa Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, kwa nini basi Madaktari, Maprofesa au hata Wakulima ambao vijiji vyenu vinaendelea mshindwe kuanzisha Blog zenu jama?

wala haihitaji fedha kwa ajili kuanzisha na kumiliki Blog, nawaombeni jamani Bogo si kwa ajili ya Waandishi wa habari ni kwa yeyote Mwenye nia ya kumiliki. msiogope jamani tafadhali msiogope.

Sunday, July 03, 2005

Junior naye Eti anasikiliza Nyeti ya Wagosi


WATOTO ni rika moja ambalo asipolelewa vyema basi ama atafanya maajabu ama madudu katika ulimwengu huu.

lakini pia utandawazi unaharibu sana watoto katika ulimwengu huu ambao wataalam wanauita ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.

Sasa Hebu angalia Junior anasilikiza Music naelewa kweli halafu mziki wenyewe wa Wagosi wa Kaya, unaitwa 'NYETI'.

HIVI KWELI TUTAFIKA JAMANI?

Tuesday, June 28, 2005

Monday, June 20, 2005

Mila Hii itawamaliza Wamasai 'Katatumaliza Jamani'

WAMASAI ni kabila moja kubwa sana, na ni kabila moja ambalo limekuwa likijitahidi kuenzi na kudumisgha mila na Destutri ya kabila hilo hapa nchini.

Licha ya kufanya hivyo wa mila zao wamekuwa wakidumisha kwa staili ya ajabu hebu kaa mkao wa kula ushangae ya Musa.

MILA hii katika kabila la kimasai inawalenga vijana ambao wamekwishaoa ambao rika lao linaitwa MORANI.

MILA hii iko hivi yaani MORANI wa kimasai anapojisikia kufanya Ngono anakwenda katika nyumba yoyote ambayo ni kijana mwenzee mwenye mke.

Kabla hajaingia ndani ya Nyumba hiyo anachomeka Mkuki wake mlangoni halafu akiingia ndani anamkuta mama mwenye nyumba wanaanza kufanya Mapenzi.

Kila mtu anajua kuwa umasaini hakuna mipira ya Kiume yaani (condoms) wanashughulika bila kutumia zana ya aina yoyote hapa.

wakati wakiwa ndani wanafanya mambo hayo Baba Mwenye Nyumba akija anakuta Mkuki uko nje ya Nyumba yake anachofanya ni kuondoka zake na kuwaacha Adam na Eva wanafaidi Tundi.

Unajua akitoka hapo anakwenda wapi? akitoka hapa na yeye anakwenda katika Nyumba nyingine ambayo ana uhakika akienda atafanya kile ambacho mkewe anafanyiwa anafika anachomeka Mkuki nje anaanza kuvunja amri ya sita bila zana!!!!!!!!!!1

Sasa fikiria ni wamasai wangapi wapo Jijini Dar Es Salaam wanafanya kazi ya Ulinzi na wafanya Ngono na machangudoa wa kule Kinondoni kwa pesa ambazo wanapata.

Wakirudi umasaini wanagawa Virusi bila kujua kuwa wanavimiiliki ndani ya miili yao kwa wake wa wenzao ambao nao watavipata bila kujua kwa wake wa wenzao.

Kamchezo kazuri sana lakini kamejaa rafu za ajabu, yani hakuna refa wala mshika kibendera na mbaya zaidi hakuna hata wale wahudumu toka msalaba Mwekundu (RED CROSS), yaani ukichezewa rafu hakuna cha huduma ya kwanza wala nini!

Sasa kama tukidumisha Mila zetu kwa staili hii ni nani atabakia katika Tanzania hii ambayo uchumi umekua kwa asilimia 4?

Wakati umefika sasa tubadilike kuendana na Karne ambayo sasa ni Sayansi na Teknolojia na hatuko kabisa katika Zama za Mawe za Kale ati ee.

NGO's, CBO's na Serikali hebu iangalie suala hili kwa ukaribu zaizi katatumaliza haka ka UKIMWI jamani kwa kudumisha mila kwa sataili hii.

Sina hakika kama TACAIDS wana habari hii hebu walifuatilie basi hili jamani.

TAKE CARE!

Friday, June 03, 2005

Kwa nini wasanii hawa washike mbele tu kunani? mnamfundisha Junior tabia Mbaya..

OO! mziki wa kizazi kipya unakua! unakua kwa vigezo gani? hebu anganlia mambo yanayofanywa na wasanii hao halafu uchangie unakua kwa vigezo gani na kiwango kipi!

kwa nini iwe mbele tu? na siyo Kwenye mataa ya Koo? kwa nini washike mbele tu tena kwenye nanihii na isiwe mgongoni au kuyakumbatia kabisa mabega?

kwa nini wasanii hawa hupendelea kushika sehemu za siri na kuziminya kana kwamba zimewakosea kwa kiasi kikubwa na wanatoa adhabu?

ndivyo mziki wa kizazi kipya unavyokua kwa kufanya mambo ya ajabu ajabu tena kwa kuiga toka kwa akina P. Diddy na wenzie kina Snoop DogDog.

Ina maana akina P. Diddy wakila V-nye-C na wao watakula vya kwao? hayo si ndo mambo ya kuiga? si twaigan kila kitu toka magharibi? Wao washike nasi tushike ? wao wakisema Maza faka nasi twasema baza faka!

wakitembea mataa ya koo nje nasisi tutembee mataaa ya koo wazi eti tu kwa kuwa P. Diddy kaacha yake nje? utamaduni huu umeanza lini kwetu Tanzania?

Mjinga atakwambia huu ni ushamba, kwani mkiimba huku mnapeperusha mikono kama mnataka kupaa mbinguni bila kuipeleka kusini mziki hautachezeka?

Si mshike basi hiyo maiki kwa mikono mikono miliwi? mbona kuna staili nyingi tu za kucheza vizuri bila hata ya kumsumbua huyo jamaa?

kama mmeshindwa kubuni staili nyingine ni bora tu muwe wastaarabu kama mnacheza ngona ya Mganda maana hii ndiyo asili yetu watanzania.

huu ni ushauri wa bure kwenu nyie vijana wa vizazi vipya, kama hamtaki mtajiju, na kushikashika kwenu huko WALAH! mtajikuta siyo ridhiki!

Mnadhani huyo jamaa anapenda kuchezewa ovyo? Mazingira, tamaduni na makuzi yetuhayako hivyokizazi kinateketea kimaadili huku wanajua kuwa wanayoyafanya si mema machoni pa watu.

makabila mengine wanapoona mnashika hivyo kwao tafsiri yao ni matusi makubwa ya nguoni sasa mnafikiri watakuja hata kwenye hayo matamasha yenu watukanwe?

Badilikeni basi vijana wenzangu kwa kuwa huo mziki wenu hata mimi naupenda sana lakini naogopa kutukanwa pale mnaposhika chini, acheni kumfundisha Junior Tabia mbaya.

wasanii wa kizazi kipya na kile cha zamani bila kuwasahau wasomaji wote mnakaribishwa kutoa maoni yenu bila jazba wala upendeleo wa aina yeyote karibuni sana!

Wednesday, June 01, 2005

Kutoka Ugogoni

Hii ndio asili halisi ya Jina 'MATONYA'

AGWEE! MATONYA ta uze ahano luluhaba ukuchemwa siukusaka kuza, Sunheee!
WEE MAMVUA hebu njoo sasa hivi kwa nini unaitwa hutaki kuja? fanya haraka!

Jina la matonya ni maaruu sana hapa nchini watu wengi wakitajia matonga huwa wanahamisha mawazo yao na kufikiria mkoa wa Dodoma yaani naanisha UGOGONI!

Matonya ina maana kubwa sana na hasa wale wenyeji wa mkoa wa Dodoma wanalifahamu hili kwa sana! yaani wanajua kuwa kama hakuna matonya lazima mwaka huo kutakuwa na njaa.

Matonya ni mvua nyingi za masika mabzo zinanyesha kwa fujo katika kipindi cha msimu wa mvua husunani katika mikoa ya kanda ya kati.

Ni kipindi cha masika yaani mvua zilikuwa zinanyesha kama hazina akili nzuri vile.

Na mara nyingi watu wa majina haya huwa ni wanaume ambao ni akina matonya, lakini kwa upande wa wanawake waliozaliwa katika kipindi hiki huitwa 'Mamvula' yaani mamvua.

Agwe Leche Duh! wala sijakutukana naanisha wee acha tu! watu wenye asili ya majina haya hutokwa sana na jasho katika muda wote wa maisha yao.

Hutokwa na jasho katika wakati wa baridi na hata wakati wa joto wao hutokwa na jasho, awe mwembamba au mnene yeye anatoka jasho kwenda mbele yaani kwa ufupi hutaniwa kuwa wana afya sana.

Sasa nafikiri mpaka hapa kila mtu ameshaelewa nini maana halisi ya jina hili kwa kuwa kila jina lina maana yake watu wengi wamekuwa wakiyakataa majina yao ya asili na kusahau kuwa huo ni utukufu wa kimila.

Jivunie kabila lako kqwa kudumisha mila ili upate baraka na heri nyingi duniani!

Tuesday, May 31, 2005

JIFUNZE KUBLOG MTANDAONI

KWA YOTE HAYO BONYEZA hapa

Kusoma nje ya Nchi sio lazima usafiri nje ya nchi yako!

HAYA jamani kwa wale waliokariri kusoma nje ya nchi mpaka upande usafiri kwa kupanda ndege na kwenda marekani au Uingereza hapana.

Unasoma nje ya nchi wakati uko ndani ya nchi, na unapata Digree kwa muda wa miezi michache kama alivyonena kaka yangu hapa Bw. R.s Miruko.
kama unabisha bonyeza hapa.

Saturday, May 28, 2005

WANAWAKE BWANA...........! YAANI AKULETEA VIRUSI NA UNAVIPOKEA KWA MIKONO MIWILI

KAMA mkeo au mpenzi wako anatoka nje ya ndoa na unajua kabisa yaani una uhakika utafanya nini?

Jibu la swali hili kwa wanaume wengi litakuwa ni lenye kuashiria maumivu kwa upande wa pili.

kwa vipi sasa?

jibu linaweza kuwa nitamwacha hapahapo au nitamwua ama tutakufa wote mimi na yeye, hayo yanweza kuwa majibu toka kwa mwanaume ambaye amefahamu hilo.ni amjibu ambayo ni ya kishujaa eh!

iwapo mwanamke angeulizwa swali hili unadhani angelijibu vipi?

bila shaka angelijibuhivi; 'nitaondoka au nitamkomesha huyo hawara yake ama shauri yake mwenyewe mimi si nitaendelea na maisha yangu' haya ni majibu muafa ya kinyonge eh!

kwa kawaida wanaume hawako tayari kusamehe kosa la kutoka nje linapofanywa na wake au wapenzi wao, ni wachache sana wanaoweza kusamehe.

sisemi kwamba hakuna wanawake ambao nao huchukulia kutoka nje kwa waume zao kama jambo lisilo sameheka, kiwango cha wanawake hao ni kidogo sana ikilinganishwa na kile cha wanaume ambao hawako tayari kusamehe uzinzi wa wake zao ama wapenzi wao.

wanaume saba kati ya kila kumi hutoka nje, tafiti zinaonyesha kuwa wanawake karibu watano katika kila kumi wanajua kuwa wanaume wao htoka nje lakini huwa hawana la kufanya, wameamua basi!

alkini wanawake wanane katika kila kumi wanajua kwamba waume zao wanatoka nje na wanachukua hatua za kupambana na hali hiyo wakiwa ndani ya ndoa zao, wakati ni mwanamke mmoja katika kila wanawake kumi ndiye huondoka kwenye ndoa ya aina hiyo. hii siyo taarifa nzuri kwa akina mama.

KUKUBALI kuishi kwenye ndoa ambapo una uhakika kabisa kwamba mwenzako anakwenda nje kutafuta kifo huku akikufuja kwa njia moja ama nyingine ni kujishusha sana, kuna wale wanaosema shauri lake kwa sababu wameshakubali kwamba wao ni watumwa wa hao wanaume bila kufikiria.

hivyo wana haki ya kupangiwa nao hata siku ya kifo, hapa wanawake na wasichana ni lazima tuwe macho na tuamke sasa tukiendelea kuishi maisha ya namna hii matokeo yake tutakuwa tunasubiria kuletewa virusi vya UKIMWI na tunavipokea kwa mikono miwili na badae tunakufa kwa ugonjwa wa Ukimwi kwa madai kuwa Mungu katutenganisha.

Wednesday, May 25, 2005

Wachungaji hawa walichunga sana Kondoo wa Bwana.!

Eee baba Mungu wabariki hawa Nguchiro wafanikiwe kwenda kwenye adhabu yako ya milee wakiwa kama kuni katikakatika ya mafiga ili waungue vyema kutokana na kuudanganya uma kuwa wao ni wachungaji wa kondoo, AMEN.

Tuesday, May 24, 2005

TLP! Ni kaaazi kwelikweli.............!!!!!!!

HAKI ya Mungu yaani Chama cha Tanzania LabourTLP kina mbwembwe kweli kweli! Zile za CCM ni cha mtoto wanawake sasa sawa na wanaume yaani wee acha tu.

ni kwamba hivi karibuni chama hicho kimemsimamisha mgombea mwenza wa urais mwanamke ambaye atakuwa akigombea nafasi hiyo na Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Augustino Lyatonga Mrema mwezi oktioba mwaka huu.

basi bwana wamemsimamisha mwanake awe mgombea mwenza wa nafasi hiyo kwa madai ya usawa unazingatiwa katika chama hicho ambacho hivi karibuni tuu kimepata ruzuku baada ya msajili wa vyama vya siasa nchini Bw. Tendwa kutangaza kuwa anakitambua chama hicho.

lakini sasa huyo mgombea mwenza anavigezo vya kuwania nafasi hiyo?

kwa kuzingatia yafuatayo wenyewe mtasema kama vigezo anavyo ama laa!

* Je Ikulu ni Maabara ya kufanyia majaribio ya uongozi?
* Ikulu ni mahali patakatifu amejitakasa?
*kazi ya urais si ya kubeba zege Bongo yake inachemka?
*utamu wa komamamnga ni komamamnga lililokomaa, amekomaa?

Angalizo: USHUZI HAUZIMI MOTO! Mnakaribishwa kuchangia maoni yenu bila woga wala Jabza na kutopendelea kwa aina yoyote, karibuni sana.

Friday, May 20, 2005

Takrima ni tatizo la Kimaumbile

Najua kila mtu ana hamu ya kulifahamu hili kwa undani kwa nini takrima iwe tatizo la kimaumbile ni maelezo machache tu hapa mda mchahe utakuwa umeelewa.

ni hivi ; kwa mujibu wa mila na desturi za kitanzania ni kwamba mtu anajikuta mwili unamuwasha kila anapokuwa anasalimiana na wenzake hapa naamanisha viongozi mbalimbali hapa kwetu tanzania.

hii inawatokea mara nyingi katika nyakati mbalimbali na hasa katika nyakati hizi ngumu za uchaguzi pale wanapojiandaa kutafuta kura katika kampeni zao.

anajikuta mwioli unamuwasha, anajikuna kwa staili ya kuingiza mkono mfukoni akitoa anatoa burungutu la pesa, anawagawiwia wapambe na wapiga kura akiwa hajitambui kabisa kuwa anawashwa anajikuna kwa staili ya aina gani.

akimaliza kujikuna anarudiwa na fahamu na kukumbuka kuwa alitoa burungutu la pesa na kuwagawia watu mbalimbali na kugunduia kuwa ametoa takrima, basi tena ndo matatizo ya kimaumbile na staili za kujikuna pale unapojisikia uanawashwa.

TAKRIMA NI TATIZO KUBWA SANA LA KIMAUMBILE SASA ANATAFUTWA DAKTARI BINGWA WA MAGONJWA YA NGOZI ASAIDIE KUTATUA TATIZO HILI KWA WATANZANIA KWA KUSHIRIKIANA NA TAKURU.

Tuesday, May 17, 2005

Itafika wakati hata Jogoo watawika Kwa Lugha ya Kiingereza!

Tangu enzi za mababu zetu watanzania tumekuwa tukijitahidi kuenzi utamaduni wetu na hasa baada ya kupata uhuru wetu mwaka 1961 chini ya Mwl J. K. Nyerere wee acha tu.

licha kuwepo kwa juhudi za kuuenzi utamaduni wetu wa kitanzania pia kupitia lugha yetu ya taifa ya kiswahili tumekuwa tukiitumia sana katika kuuenzi utamaduni huu kuanzia katika shule za awali hadi vyuo vikuu.

kutokana na watanzania wengi kujitahidi kuendeleza zoiezi zima la kuuenzi utamaduni wao kumekuwapo na vikwazo kibao ambavyo vimekuwa vikiwafanya watanzania hawa kushindwa kuendelea katika suala la kuuenzi utamaduni kutokana na baadhi ya viongozi wao kukazia kutumika kwa lugha ya kiingereza.

kutokana na watanzania kukaririshwa kuwa kiingereza ni lugha ya kimataifa na kutokana na tanzania kufikiria tena kuingia katika shrikisho la jumuiya ya nchi za afrika mashariki hapa watanzania wamekuwa wakichanganyikiwa sana.

kinachowachanganya ni kuhusiana na hiyo lugha wanayoambiwa kuwa ni ya kiamtaifa kama huijui huwezi hata kufanya biashara ya kuku nje ya nchi, kikubwa zaidi kinachowachanganya watanzania wanaoishi kule mvumi kuhusiana na wao kufanya biashara nje ya nchi wakati hata 'kiswakigo' (kiswahili Kigogo) chenyewe kimepita kushoto.

lakini kinachowachanganya zaidi ni suala la kuwafundisha mbuzi wao wanaotegemea kwenda kuwauza nje ya tanzania jinsi ya kulia kiingereza au jinsi ya kuwafunda kuku wao jinsi ya kuwika kiingereza wanapokuwa katika masoko nje ya Tanzania.
Itakuwa ngumu sana kufamnikiwa katika suala la kuuenzi utamaduni wa mtanzania kupitia katika lugha ya taifa ya kiswahili huku viongozi wakisisitiza kuwa kiingereza ni lugha ya kiamataifa, umefika wakati ambapo mataifa mengine waambiwe kuwa kiswahili ni lugha ya kiamataifa.

ili nao waanze kuwafundisha kuku wao kuwika kokoriiiko yaani kwa kuwika katika lugha ya kiswahili au waanze kuwafundisha mbuzi wao kulia kwa lugha ya kiswahili Meeemeeeee! ili tufikikie malrngo ya kuuenzi utamaduni kama wao walifanikiwa.

Monday, May 16, 2005

Ukitaka kwenda mbinguni lazima upitie nji hii hapa

Ni kuzuri sana, lazima upapitie hapa kabisa usipopitia hapa ujue unakwenda kwingine. Kong'oli hapa!

Ndoa ni kazi Ngumu lakini ni Muhimu, kwa nini wengine hawaowi au kuolewa?

Ndoa ni agano linalowekwa kati ya mwanaume na mwanamke wabatizwa mbele ya Mungu ili wawe mke na mume.

Kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu, agano hili linawafanya wabatizwe wawe mwili mmoja wakishiriki haki zote za ki-ndoa pamoja na mafao ya kijamii yatokanayo na hali ya ndoa.

sasa ni kwa nini wengin hawaowi wala kuolewa, Bofya hapa!

He! Kumbe kuna watu wanakunywa pombe kila siku lakini hawafahamu bei yake........

Ni ngumu kuaminishwa lakini utakaposhuhudia ni lazima ukubali kuwa ni kweli yanatokea.

hii kwa wale wahudumu wa sehemu zinazouzwa Pombe yaani 'Bar wanalitambua sana hili na wala sio geni kwao kutokana na uzoefu wa kazi yao ya kuuza bia kwa watu mbalimbali.

wahudumu wao ambacho hujali ni kulipwa pesa zao haijalishi pesa hiyo ni ya wizi au ya kuhongwa kitu ambacho kimekuwa kikiwagharimu wanunuaji au walipaji wa vunywaji husika.

hapa kubwa ninalolizungumzia ni kuhusiana na tabia ya baadhi ya watua mabo kila mda ukikutana naye kila muda yeye amelewa tu halafu kabla ujamuuliza utasikia anakwambia niko pombe anadhani ni sifa kubwa mbele ya watu anaowambia.

lakini cha kushangaza ni kwamba mtu huyohuyo ukimuuliza umekunywa ngapi kwa sauti kubwa atakujibu harakaharaka nimekunywa kumi, na ukimuuliza ni sawa na kiasi gani cha pesa alichotumia utamuona anainama chini kana kwamba anafikiria kitu cha maana badala yake anakujibu SIJUI.

NI hatari sana kwa wale wenye tabia hii hususani ni akinaada ambao kutwa yuko pombe ukimuuliza bei ya bia moja hajui ni kiasi gani akian kaka nao tabia hii ni hatari sana zaidi kuliko kwa akina dada, lakini haya si mawazo yango hata R.S analitambua hilo.

Hebu tuweni na ustaarabu jamani hata kama unapewa ofa kila siku basi siku moja pita mwenyewe bar ujaribu kuulizia bei tu ya bia kama unavyofanya kwenda dukani kuulizia bei ya kiatu au nguo ili uwe na uhakika wa ofa unazopewa mtaani.

Monday, May 09, 2005

Ni kweli kuwa CCM ya Mkapa ni tofauti ile ya Nyerere?


haki yangu Mungu siasa ni mchezo mtamu sana, lakini mambo yanapokugekia utatamani ardhi ipasuke uingie ndani ili watu wengine wasikuone, wapinzani nao wana mambo Soma hapa

Wengine walishehekea hivi Siku ya mama!

Tarehe 8 May kila mwaka duniani kote husherehekea siku ya mama Yaani Mothers Day!

hapa kwetu Tanzania watanzania nao pia walisherehekea siku hii kwa furaha kubwa ikizingatiwa siku hii iliangukia katika siku ya Jumapili ambayo ni siku ya mapumziko ya mwisho wa wiki.

wengine walisherehekea siku hii kwa kuwashukuru mama zao kuwaweka hapa duniani kwa kuwazaa, kuwalea na kuwapatia kila kilicho mahitaji yao na kuwafikisha hapo walipo sasa.

wengine waliwapatia mama zao zawadi mbalimbali ikiwemo kadi, maua na zawadi nyinginezo nyingi kwa ajili ya kuonyesha upendo wao halisi kwa mama.

lakini kwa upande wa wa wafanyabiashara hali kwao ilikuwa tofauti na wengine kwa kuwa wafanyabaishara wao walikuwa wakifanya biashara kwa kuuza kadi za siku ya mama na maua kwa ajili ya siku hiyo.

mwanzilishi wa siku hiyo Bibi. Anne amekilaani kitendo hicho cha kufanya biashara kwa kusema kuwa kuwa lengo la siku hiyo halikuwa kufanya baishara kama wanavyofanya sasa watu wengi hapa duniani.

anasema kuwa lengo la kauzishwa kwa siku hiyo ni kuwapongeza akina mama ambo walikuwa wakiwapokea waume zao ambao walikuwa wakirejea kutoka vitani ambao kabla ya kuondoka waliawaacha akina mama hao wengine ama wakiwa na watoto wadogo ama mimba ambazo akina mama hao pamoja na kupata shida zote za upweke waliweza kuwalea watoto wao na kaundaa mapokezi kwa ajili ya kuwapokea waume zao ambao walikuwa wakitoka vitani.

upendo huu waliouonyesha akina mama hawa ulisababisha kuanzishwa kwa siku hii muhimu sana na siyo kwa ajili ya kufanya baishara kama ilivyo sasa. HONGERENI AKINA MAMA!

'FIRST LADY' Huyu hakupata kitchen Party kabla ya Kuingia Ikulu?



KILA mtu anaamini kuwa Ikulu ni mahali patakatifu na kila anayeingia Mahali hapo alzima awe ametakaswa kabla hajaingia, licha ya kuwa ni ngumu mtu kutakaswa kabla hajafa.

suala la kujitakasa pia ni zuri na hasa kwa akina mama ambao wana madaraka makubwa ya kuwaongoza wenzao au akina mama ambao waume zao wana madaraka makubwa hii ikiwa ni pamoja na kuwa mke wa rais.

nawapa pole sana wenzangu wakenya, hapa naamanisha watu wote wanaoishi kenya Afrika mashariki hii ambayo tunategemea kuwa na Jumuiya ya afrika mashariki kwa kuchangia kila kitu hususan katika masuala ya biashara.

pole hii hasa ni kwa akina mama wa kikenya, nawapa pole sana hawa kwa kuwa mke wa rais waoamekuwa akifanya mambo ya ajabu ikiwa ni pamoja na kushinikiza mumewe kufanya mambo ya ajabu ajabu kutokana na mumewe kuwa na cheo cha juu cha utumishi kuliko vyeo vingine hapa afrika.

mama huyu licha ya kufanya mambo ya ajabu hivi akribuni alitoa kali baada ya kuvamia chumba cha habari cha gazeti moja la nchini kenya akitaka kuombwa radhi kutokana na gazeti hilo kumuandika.

licha ya kuvamia chumba hicho cha habari pia mama huyo alimpiga vibao mpiaga picha wa gazeti hilo kwa madai kuwa alimpiga picha!

sasa mablogist wanawake wenzangu kwewli hii ni haki? mwanamke mzima mwenye akili timamu na mumeo ni mtu mwenye madaraka ya juu unafanya mambo kama mtoto mdogo anayesoma vidudu?

poleni sana akina mama wa kenya huyu mwanamama amewadhalilisha sana akinamama wa kenya kwa tabia yake hiyo ya ajabu kwa kufanya hivyo watu wa mataifa mbalimbali wamefikiria kuwa wanawake wa kabila lake wote wako kama mama huyo alivyo. pole sana First Lady! milango iko wazi kwa ajili ya kuchangia maoni yenu kuhusiana na tabia ya mama huyu wa ajabu karibuni wanablog.

Saturday, May 07, 2005

Kaguo alamba Ugombea wenza 2

kutokana na sababu za kiufundi habari hii haikuweza kusoma vilivyo lakini sasa mambo yanaenda kama yalivyopangwa.Kong'oli hapa

Thursday, May 05, 2005

MAPAPARAZI wapewa vitambulisho vya Wahudumu!

Waandishi wa habari ni watu muhimu sana hapa nchini na duniani kote kwa ujumla na wengi wamekuwa wakiita fani ya uandishi wa habari kuwa mhimili wa nne!

lakini watu hawa wamekuwa wakionekana kuwa hawana maana sana na hasa pale wanapoalikwa katika shughuli mbalimbali za kitaifa.

Ni hivi karibuni mjini Dodoma kulimalizika tukio kubwa ambalo lilikuwa linakamilisha neno kutimia ambapo wana CCM walikuwa wakiteua mgombea urais ambaye wengi wanaamini huyo ndiye rais wa awamu ya nne.

katika mkutano mkuu huo maalum wa CCM wageni wengi toka ndani na nje ya nchi walialikwa kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wakiwemo waandishi wa habari toka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

licha ya kualikwa kwa wageni wengi na waandishi pia, wageni hao walitafutiwa mahali pazuri pa kulala na kupewa kadi maalum za kuingilia katika ukumbi wa mikutano wa CHIMWAGA.

kinyume na wageni wengine waandishi wa habari hawakupewa uzito kama ilivyokuwa kwa wageni wengine ambao walialikwa kuhudhuria Mkutano huo na badala yake walionekana kama wafanyabiashara wa nguo toka mikoani.

siku ya mkutano baadhi ya waandishi wa habari walionekana kukosa kabisa kadi hizo maalum ambazo walitakiwa kuwa nazo na kuwaruhusu kuingia katika mkutano huo maaluma ambao ulikuwa na ulinzi kupita kiasi.

baadhi ya waandishi wa habari na wapiga picha ambao walibahatika kunusa milango ya ukumbi huo walipata kadi za uhudumu wa Vinywaji na vyakula ambazo zilkuwa zinatumiwa na wauzaji wa vyakula na vinywaji nje ya ukumbi huo.

hii iliniuma sana, mbaya zaidi ni pale matukio muhimu yaliyokuwa yakitokea ndani ya ukumbi huo yalikopokuwa yanafanyika wapiga picha na waandishi wa habari walitakiwa kushuhudia ili kuwapa taarifa wananchi ambo wako tandahimba.

ilikuwa ngumu kwao kuingia kutokana na vitambulisho vyao kuwaruhusu waandishi na wapiga picha kuishia nje ya milango ya ukumbi huo.

kilichokuwa kinagomba hapa ni kwamba baadhi ya maafisa wa usalama walikuwa wakiwaambia waandishi hawa kuwa "nendeni mkawahudumie huko nje huku ndani tuko kamili"

licha ya kunyimwa vitambulisho pia walifukuzwa katika nyumba za kulala wageni amabzo walikuwa wamefikia kwa madai kuwa CCM ilikuwa imezikodi nyumba zote kwa ajili ya kufikia wajumbe wa Cma hicho.

hii inaonyesha ni jinsi gani waandishi wa habari wasivyothaminiwa katika jamii hususan na baadhi ya viongozi wa Chama cha mapinduzi katika idara ya habari.

CCM kama hamuyawezi waachieni Idara ya habari maelezo watayamaliza wao bila kufanya hiyana kama mliyofanya katika mkutano wenu mlitukwaza sana.

Tumewasamehe na tumemkemea Pepo mchafu aliyemo nsdani ya chama chenu katika jina la Yesu ashindwe na asiendelee kuwepo! AMINA.

Ni moshi wa kijani lakini sio wa Mjomba.............!

HAYAWIHAYAWI sasa yamekuwa, jana mosho wa kijani ulifoka katika ukumbi wa Chimwaga na kuwamwaga wale 2 ambao walitakiwa kumwagwa haraka sana kabla Jogoo halijawika.

hatimaye jana neno likatimia! shangwe na vilelegele vifijo na Nderemo nguo za kijani, moshi wa kijani hii ilikuwa ikimaanisha sasa Imekwisha.

kilichonitia wasiwasi ni pale Moshi ule wa kinai uliotoka na kuonnyesha aliyekuwa amechaguliwa ni mwingine siyo mjomba wangu! hapa ilikuwa ni ngumu kuamini lakini baadaye fahamu ziliponirudia nikaamini kuwa ni kweli hakuwa Mjomba.

lakini kwani huyo na mjomba wana togfauti gani hapa nilijiuliza na kukosa jibu kabisa lakini nilipomuuliza Binamu akaniambia kuwa eti mjomba alikuwa Mzee sana kuliko huyo mteule.

nikamuuliza Binamu kwani Ikulu kuna kazi za kubeba Zege? akanijibu kuwa hata kama kazi si za kubeba zege lakini huu ni muda wa vijana kuonyesha ujana wao katikia wakati wao wa ujana hususan ni kipindi hiki.

sikuishia hapo nikamuuliza tena; kwani ukienda katika kijiji ambacho umgeni sana utatafuta kijana maarufu au Mrembo maarufu na kuuliza shida yako?

akajibu hapa, nikamuuliza tena utumtafuta nani na kumuuliza? akijibu; nitamtafuta Mzee maarufu na kumuuliza.

hapo nikaridhika kumoyo! nataka kukwambia Binamu kuwa sasa kwa taarifa yako Mjomba amekata rufaa! na Ikulu hakuna kazi ya kubeba Zege na utamu wa embe ni lile ambalo limeivia juu ya mti siyo la kuvundika.

Kaguo alamba ugombea Mwenza

Waandishi wa habari nao hawako nyuma kwa Vituko na hiki ni kimojawapo kati ya vituko hivi! Soma hapa

"Hata nisipochaguliwa nitarudi kuwashukuru"

Hapa namnukuu aliyekuwa mmoja kati ya wale wanaiomba CCM kumteua kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho alipokuwa akirudisha fomu ya kuomba baraka hizo

Mgombea huyu alisema kuwa iwapo hatobahatika kupata nafasi hiyo ya kuteuliwa na kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho basi angerudi katika mikoa yote 26 aliyozunguka wakati akiomba wasdhamini kwa ajikli ya kumdhamini katika suala zima la kupata baraka za kuteuliwa kuwa mgombea urais.

alisema kuwa angerudi na kuwashukuru wale wote waliomdhamini na kuwataarifu matokeo juu ya kile kilichotokea katika uteuzi huo.

swali? je ni kweli atafanya hivyo!

nafikiri itakuwa ngumu sana kwanza bado anazo nguvu za kwenda huko kuzunguka na kuwatafuta tena wadhamni wake na kuwakatia takrima kama alivyofanya hapoa awali alikwenda kuwabembeleza kwa ajili ya udhamini?

nasubiri sana huu wimbo urudiwe kuimbwa na mwasiasa huyu ambaye alipokuwa akiyasema haya alionyesha ujasiri wa hali ya juu kana kwamba alikuwa an uhakika wa kuwa mteule katika nafasi ya kuwa rais mgombea.

haya tunakusubiri kwa hamu sana baba! wadhamini pia wana hamu ya kujua yaliyokusibu mpaka ukachinjwa na kutupiliwa mbali.

WELCOME BACK utupe FEEDBACK!

Monday, May 02, 2005

Kuzirai ni Muhimu lakini Kulia kwa Wabarabaig ni Mwiko

Najua huwezi kuamini lakini jinsi hali inavyooneka ndivyo itakavyokuwa, ni ngumu kuamni lakini ukweli utabaki kuwa palepale, hao 10 kati yao wengi watalia, lakini inawezekana 9 tu ndio watakaolia huyo 1 itakuwa ngumu KULIA anaweza akazirai na kupoteza fahamu lakini asidondoshe hata chozi kutokana na imani za huko kwao Mbulu.

Hayo yatakuwa ni matokeo tu na ukweli utabaki kuwa palepale!

TOP 5 wa sensitine ndogo ya Nec hawa hapa!

Haki ya Mungu yaani huwezi kuamini mambo CCM yaani chama cha mapinduzi, watu wote sasa masikio yao na akili zao zote zimeelekezwa mjini Dodoma kwa ajili ya kujua ni nani atakayepigana kiume kufa na kupona kwa ajili ya kumrithi Mkapa.

Kubwa ambalo hata wenyeji wa mkoa wa Dodoma ambao pia nao ndi wanaishi hapa mbado wana hamu ya kuwafahamu hao waliofanikiwa angalau kuonja kidogo hayo ambayo kwa pia wanahisi ni mafanikio ya kuanza safari ya kwenda Sensitine Kubwa ya Chimwaga.

akina mama nao hawako nyuma, wako msatari wa mbele kwa ajili ya kufanikisha akina baba ambao walijitokeza katika kuonja majaraibio ya kinyan'ganyiro hicho wanafanikiwa na wao kuitwa 'FIRST LADY' licha ya kuwa wao waliogopa kluchukua fomu na kuongozana na waume zao ambao hapo baada nafikiri wangeitwa 'FIRST GENTLEMAN'

mpaka sasa wachezaji 11 wako uwanjani wakiongozwa na golikipa Babu Ushindi ambaye kwa mujibu wa wataalam wa mambo ya siasa anatisha kimsingi.any way kesho utawafahamu hao TOP 5! USIKOSE!

Sunday, May 01, 2005

Wanawake wasubiri 'moshi wa kijani' Chimwaga

Licha ya ukweli kuwa hakuna hata mmoja aliyejitokeza kwa ajili ya kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya CCM, bado wanawake nchini Tanzania, kama walivyo Watanzania wengine watakuwa wakisubiri kwa hamu kujua kuwa baraza la mapapa wa CCM litafukiza moshi wa aina gani baada ya vikao vyao vitakavyofanyika katika siku tatu zijazo mjini hapa.

Kwamba kutatoka moshi wa aina gani, hilo sio swali ambalo mtu anaweza kulijibu kwa haraka sana hasa kwa kuzingatia kuwa karibu wagombea wote wana nafasi sawa ya kuweza kushinda licha ya tambo, mbwembwe na madoido ya hapa na pale yaliyoshuhudiwa toka kwao toka walipochukua hadi kurudisha fomu.

Je ni moshi wa kijani, wa njano, kijani na njano, moshi mwekundu kama alivyosema kakayangu Kulangwa au ni cheche kama alivyosema kaka yangu Rama? Swali hili litajibika hivi karibuni baada ya baraza la mapapa wa CCM kukutana pale 'Sestine' yao (Chimwaga). Tuombe kheri na Mungu atuongoze.

Saturday, April 30, 2005

Kutoka Ugogoni

Namaanisha kutoka kati kati ya Tanzania, katika mkoa unaokwenda kwa jina la Dodoma (zamani Idodomya), mkoa ambao toka miaka ya kupata uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania), viongozi wetu wamekuwa wakiota kuufanya makao makuu ya nchi hii, ingawa ndoto hii ya viongozi wetu wakuu, imeendelea kuwa kuukuu kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Naam, huko ndiko anakoibukia binti huyu wa Kitanzania, ambaye kwa jitihada nyingi za binafsi na za washauri mbalimbali, ameamua kuvamia ulimwengu wa Blogi. Ujumbe wake kwako ni kuwa, anajua kwamba itamchukua muda sana kuweza kufikia hatua za juu sana katika teknolojia hii, lakini haidhuru anaamini ipo siku atafika kwa msaada wako na wa wengine pia.

Hii ni nuru kutoka kwa Wagogo, kabila kuu katika ukanda anakotoka mwanablogi huyu, japo nalo pamoja na kuwa kabila kuu, bado hali yao imeendelea kuwa kuu kuu kwa miaka nenda rudi. nani ajuaye, huenda siku zao za ukombozi ndio zimeanza leo hii, tusubiri tuone.

Shukrani kwa wote mliokuwa na hamu ya kuona mtu kama mimi naibuka kwa ajili ya ninyi kuniunga mkono.