Saturday, August 20, 2005

Nikusikie tena unatishia watu Amani!


Inasemekana Vyama vya upinzani vinafanya fujo makusudi kutokana na wagombea wa Vyama hivyo kujua kuwa havitashinda katika uchaguzi Mkuu ujao.

Lakini kwa mujibu wa Wachunguzi wa masuala ya Siasa wanasema kuwa ni katika kujitetea tu ndio maana vyama hivyo vinafanya hivyo,

Je wewe Msomaji wa Blog hii una maoni gani? unafikiri ni kwa nini inakuwa hivyo? weka maoni yaklo hapa ili unisaidie kuelewa ni kitu gani kifanyika na kwa malengo hani hasa, unakaribishwa kuweka hoja zako bila jaza wala upendeleo wa aina yoyote.

Karibuni.

2 comments:

Ndesanjo Macha said...

Nadhani ukifuatilia kila tukio la fujo ambalo limewahi kutokea toka siasa ya vyama vingi kurudishwa Tanzania, utagundua kuwa karibu vyama vyote vikubwa vimewahi kuhusika kwa namna moja au nyingine katika fujo. Lakini tunajua pia kuwa imetokea mara nyingi sana wanachama wa upinzani wanashiriki kwenye fujo baada ya kuchochewa na wale "askari wa kuleta fujo" (FFU). Ukiacha vyama, ukija kwenye jeshi, mara nyingi sana jeshi hili limeleta fujo na kuumiza watu na kuharibu mali mitaani. Acha hiyo, familia nyingi sana Tanzania zinaogelea kwenye bahari ya fujo na unyama. Mtoto akikosa anapigwa kama mbwa wa mtaani, mama akichelewa kupika anashushiwa masumbwi utadhani amekuwa mfuko wa kufanyia mazoezi wa bondia aliyechacha Tyson. Gerezani nenda uone...eti wanasema ni mahali pa kurekebisha tabia. Zanzibar kule wanaita chuo cha mafunzo. Mazingira ya gerezani yamejengwa juu ya saikolojia na mahusiano ya fujo na ukandamizaji. Lakini pia wakati viongozi wetu wanapoongelea fujo, wanataka tuelewe fujo kwa maana moja tu. Kumbe hata kunyimwa haki za kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni ni aina ya fujo. Unaponyimwa haki ya kutoa mawazo yako, kwa mfano, hiyo ni fujo dhidi ya nafsi na saiki yako. Kisaikolojia unakuwa kwenye mateso pengine makubwa kuliko yale ya mwananchi aliyetupiwa chungwa na mfuasi wa chama cha wapinzani.

Reggy's said...

Siamini kuwa vyama vya upinzani Zanzibar ndivyo vinaleta fujo kwenye visiwa vya karafuu. Imani yangu inanituma kuwa CCM siku zote ndiyo inayoleta fujo, lakini kwa jinsi ilivyojijengea mazingira ya kuogopwa, kutokuguswa, fujo zake zinahamishiwa kwa wapinzani. CCM ikifanya jambo Zanzibar, inawahi kuitangazia dunia kupitia vyombo 'vyake' vya serikali, ili CUF ionekane ndiyo balaa. Ingawa CUF siwatetei saaaaaana, lakini naamini fujo kubwa za kusikika, kama kuua watu zilifanya na serikali ya CCM.